Tuesday, 26 August 2014

JINSI YA KULIMA UYOGA NA KUONGEZA KIPATO CHA ZIADA



Uyoga ni chakula kizuri sana na chenye virutubisho vingi vinavyohijika katika mwili wa mwanadamu, Wataalumu wengi wa afya na tiba wanautumia katika kutibu magonjwa mbalimbali kwa mwanadamu, Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa uyoga unavitamini za kutosha pamoja na protini.


 Miaka ya karibuni, utaalamu wa kuotesha uyoga umeanza hapa Tanzania baada ya watu kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine ya zao hilo. Kwa kuwa uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake pia hutofautiana katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, pia uyoga una soko kubwa na unaweza kumuongezea kipato mkulima kwa kuuza kwa kuwa unahitajika sana na watu wa lika zote pia unaweza kutumiwa kwa namna mbalimbali,kama vile chakula nk.



 Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua jinsi ya kuulima inavyopaswa na pia ni wachache wanaoweza kutofautisha aina mbalimbali za uyoga na upi unafaa kuliwa na upi haufai kwa kuliwa. Mama Witness M. Marwa wa Mazimbu Morogoro Tanzania ni kati ya wakulima wachache wanaujua jinsi ya kulima uyoga kitaalam, pia anajua kutofautisha uyoga unaofaa na usio faa kwa kulimwa. Pia ni kati ya wakulima wazoefu katika manispaa ya morogoro ambao wananufaika na kilimo cha uyoga.


Anaanza kuueleza kuwa ,  kwa Tanzania aina zinazofaa ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C. Aina hizi za uyoga pia uhitaji hali ya unyevu hewani (moisture) wa kiasi cha asilimia 75%. Kwa mfano uyoga aina ya mamama.

                            Mfano wa Ujenzi wa banda uyoga



















UOTESHAJI WA UYOGA


Ikiwa unahitahitaji kuanza kuotesha uyoga, inabidi kwanza uwe na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki ni vyema kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima










Mara Nyingi mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au jamii

nyingine za uyoga ambazo haziliwi.



UHIFADHI WA UYOGA

i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka kwenye mifuko ya nailoni liyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.

SOKO LA UYOGA
i) Watu wengi hupenda uyoga mbichi uliotoka shambani wakati huo huo kama kitoweo, kwa kutumia kama nyama, samaki, au kama kiungo.
ii) Unaweza kuuza uyoga mbichi kwa bei ya shilingi 8000/= hadi 15000/= kwa kilo kwa uyoga aina ya mamama.
Pia unaweza kuuza nje ya nchi ikiwa uyoga wako ni kiasi kikubwa na uko katika viwango vinavyo kubalika kimataifa.


MAMBO YA KUZINGATIA
Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio
karibu nawe.

Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.

Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha
unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.

Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.

Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa
vimelea.

Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji. Unaweza kupata faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga,

FAIDA ZA UYOGA:-
Lishe kama protini inayolingana na ile ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde. Pia utapata vitamini B, C, na D, na madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.

Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.

Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga, na baada ya kilimo cha uyoga yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.

Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.

  Kilimo hiki ni njia nyepesi ya kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika na pato lake ni kubwa, hivyo kupunguza utegemezi kwa familia na umaskin pia hasa kwa atayetilia maanani na mkazo katika kulima uyoga. 

Makala hii imeandikwa na Magesa Melkory M, Kwakushirikiana na Mama Witness M. Marwa mkulima wa uyoga MOROGORO TANZANIA.