Thursday 26 June 2014

SUA YAWA YA KWANZA KUGUNDUA CHANJO YA UGONJWA WA NDUI DUNIANI





ugonjwa wa ndui kwa kuku, baada ya siku 11 unavyoonekana kwa kuku

Tanzania imeingia katika vitabu vya kihistoria ya tiba baada ya Profesa Philemon Wambura kugundua chanjo ya ugonjwa wa ndui kwa kuku ambayo imetambuliwa kimataifa.Chanjo hiyo iitwayo ‘Fowl Pox TPV-1 strain,’ iliyofanyiwa utafiti kwa miaka 10 na ya kwanza kugunduliwa duniani, itaanza kutumika Afrika na dunia nzima hivi karibuni.

Wakati wa utiaji saini wa makubaliano na kampuni ya kimataifa  inayotengeneza dawa na chanjo mbalimbali za mifugo, MCI Sante Animale ya Morocco, Profesa Wambura alisema chanjo hiyo ni ya kwanza kukubalika kutumika kuzuia ugonjwa wa ndui ya kuku na ni rahisi kutumia ukilinganisha na chanjo nyingine zilizowahi kufanyiwa majaribio.“Ni fahari kwa Tanzania kuwa mgunduzi wa kwanza wa chanjo hii duniani, ni chanjo yenye ubora wa hali ya juu  na matumizi yake yataongeza uzalishaji wa kuku na kuongeza kipato,” alisema Profesa Wambura ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Tiba ya Wanyama wa Chuo cha Kilimo Sokoine (SUA).

Profesa Wambura alisema tofauti na chanjo nyingine, hiyo inaweza ikawekwa kwenye chakula au maji ya kunywa bila kupata usumbufu wa kuwakamata mmoja mmoja na kuweka dawa machoni kama ilivyozoeleka.Alisema chanjo hiyo ina sifa kubwa ya kuvumilia joto, jambo linaloifanya kuwa ni rafiki wa mazingira ya vijijini ambako hakuna umeme na ina uwezo wa kutambua iwapo kuku ana virusi vya ugonjwa wa ndui kwa kutumia damu ya kuku mwenyewe.

“Madhumuni yetu ni kuhakikisha chanjo hii inapatikana kwa bei nafuu ili hata wananchi wa kawaida wanufaike. Ndiyo maana itazalishwa kwa wingi ili iuzwe kwa bei nafuu,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Hassan Mshinda alisema ni fahari kubwa kuwa kazi ya mtafiti wa Kitanzania imeonekana na mataifa ya nje, jambo ambalo linatoa ari kwa watafiti wengine kufanya kazi zaidi.Alisema mradi  huo wa chanjo ya ndui ya kuku uliogharimu Sh205 milioni ni wa kimataifa na chanjo hiyo itasambazwa duniani kote kwa ushirikiano wa Costech na Kampuni ya MCI.

“Ni vizuri sasa tafiti za Kitanzania zinatumika badala ya kuhifadhiwa kwenye makabrasha bila faida yoyote. Ni kazi ya kujivunia hasa,” Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji wa Biashara wa MCI, Dk Baptiste Dungu alisema kampuni yake imefanya kazi na Profesa Wambura na kugundua kuwa utafiti wa chanjo yake una manufaa makubwa kwa sababu ni wa kwanza duniani.

Kwa kawaida ugonjwa wa NDUI YA KUKU, kuku huonekana na vipele vya rangi ya kijivujivu, kwenye ngozi yake, hasa kwenye upanga wa kichwa.


habari hii inapatikana pia, http://magesam.blogspot.com/