ugonjwa wa ndui kwa kuku, baada ya siku 11 unavyoonekana kwa kuku
Tanzania imeingia katika vitabu vya kihistoria ya tiba
baada ya Profesa Philemon Wambura kugundua chanjo ya ugonjwa wa ndui kwa kuku ambayo
imetambuliwa kimataifa.Chanjo hiyo iitwayo ‘Fowl Pox TPV-1 strain,’ iliyofanyiwa
utafiti kwa miaka 10 na ya kwanza kugunduliwa duniani, itaanza kutumika Afrika
na dunia nzima hivi karibuni.
Wakati wa utiaji saini wa makubaliano na kampuni
ya kimataifa inayotengeneza dawa na chanjo mbalimbali za mifugo, MCI
Sante Animale ya Morocco, Profesa Wambura alisema chanjo hiyo ni ya kwanza
kukubalika kutumika kuzuia ugonjwa wa ndui ya kuku na ni rahisi kutumia
ukilinganisha na chanjo nyingine zilizowahi kufanyiwa majaribio.“Ni fahari kwa Tanzania kuwa mgunduzi wa
kwanza wa chanjo hii duniani, ni chanjo yenye ubora wa hali ya juu na
matumizi yake yataongeza uzalishaji wa kuku na kuongeza kipato,” alisema
Profesa Wambura ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Tiba ya Wanyama wa Chuo cha
Kilimo Sokoine (SUA).
Profesa Wambura alisema tofauti na chanjo nyingine, hiyo
inaweza ikawekwa kwenye chakula au maji ya kunywa bila kupata usumbufu wa
kuwakamata mmoja mmoja na kuweka dawa machoni kama ilivyozoeleka.Alisema chanjo hiyo ina sifa kubwa ya kuvumilia joto, jambo
linaloifanya kuwa ni rafiki wa mazingira ya vijijini ambako hakuna umeme na ina
uwezo wa kutambua iwapo kuku ana virusi vya ugonjwa wa ndui kwa kutumia damu ya
kuku mwenyewe.
“Madhumuni yetu ni kuhakikisha chanjo hii inapatikana kwa
bei nafuu ili hata wananchi wa kawaida wanufaike. Ndiyo maana itazalishwa kwa
wingi ili iuzwe kwa bei nafuu,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech),
Dk Hassan Mshinda alisema ni fahari kubwa kuwa kazi ya mtafiti wa Kitanzania
imeonekana na mataifa ya nje, jambo ambalo linatoa ari kwa watafiti wengine
kufanya kazi zaidi.Alisema mradi huo wa chanjo ya ndui ya kuku
uliogharimu Sh205 milioni ni wa kimataifa na chanjo hiyo itasambazwa duniani
kote kwa ushirikiano wa Costech na Kampuni ya MCI.
“Ni vizuri sasa tafiti za Kitanzania zinatumika badala ya
kuhifadhiwa kwenye makabrasha bila faida yoyote. Ni kazi ya kujivunia hasa,” Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji wa Biashara wa MCI, Dk
Baptiste Dungu alisema kampuni yake imefanya kazi na Profesa Wambura na
kugundua kuwa utafiti wa chanjo yake una manufaa makubwa kwa sababu ni wa
kwanza duniani.
Kwa kawaida ugonjwa wa NDUI YA KUKU, kuku huonekana na vipele vya rangi ya
kijivujivu, kwenye ngozi yake, hasa kwenye upanga wa kichwa.
habari hii inapatikana pia, http://magesam.blogspot.com/
habari hii inapatikana pia, http://magesam.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment