
Ulishaji
Kuku wa kienyeji wanaweza kulishwa kwa
kumia mahindi, mchele, na mabaki ya ugali. Vyakula hivi ni lazima vikaushwe
vizuri na kusagwa vizuri. Ulishaji ni lazima ufanyike katika sehemu safi au kwa
kutumia vyombo vilivyotengenezwa maalumu kwa ajili ya kulishia kuku.
Banda
Aidha kuku wawe wa kienyeji au wa kisasa,
wanahitaji kuwa na banda zuri kwa ajili ya malazi na kuwalinda. Wanahitaji chumba
chenye nafasi ya kutosha na kinachopitisha hewa ya kutosha. Ni lazima kuwawekea
fito kwa kuwa ndege hupenda kupumzika juu ya fito. Ni lazima banda la kuku
lifungwe vizuri nyakati za usiku ili kuzuia wanyama wanaoweza kuwadhuru kuku.
Ni lazima liwe safi wakati wote ili kuzuia magonjwa kama vile mdondo na
mengineyo. Usitumie pumba za mbao au nguo kuukuu kwenye viota vya kutagia kwani
huchochea kuwepo utitiri na funza wa kuku. Inashauriwa kutumia mchanga laini.
Maji ya kunywa
Kuku wapatiwe maji safi. Ni
lazima kuangalia mara kwa mara na kuyabadilisha maji. Kamwe usiwape kuku maji
machafu.
Chanjo
Chanjo kwa mifugo ni lazima ili kuzuia
mashambulizi ya magonjwa. Magonjwa yaliyozoeleka ni kama vile Mdondo, Kideri,
Ndui ya kuku, na homa ya matumbo (typhoid). Chanjo kwa kawaida hutolewa mara
moja kwa kila baada ya miezi miwili.
Uwekaji wa kumbukumbu
Kumbukumbu zijumuishe aina
ya ulishaji, namba ya uzalishaji, muda wa mwisho wa matumizi, kiasi cha
malisho kwa kila siku, idadi ya vifo, na idadi ya mayai
yaliyozalishwa.
Mwanzoni unahitaji nini?
Wafugaji walio wengi wanauliza wanahitaji nini katika hatua
za awali ili kuweza kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku. Hii itategemea aina ya
kuku uliochagua kufuga.
Ni busara kuwa na vifaa muhimu vinavyohitajika na viwe
katika hali ya usafi kabla ya kuweka kuku bandani mwako. Kama unaanza na
vifaranga, vifuatavyo ni vifaa muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya vifaranga
200.
• Tengeneze banda zuri lenye joto na hewa ya
kutosha wakati wote.
• Vyombo vinne (4) vya kunyweshea maji, hii ni katika wiki 2
za mwanzo na uongeze vyombo taratibu kulingana na kuku wanavyokua.
• Vyombo vinne (4) vya kulishia chakula, na viongezeke
kulingana na kuku wanavyokua.
• Matandazo makavu na safi, inaweza kuwa maranda au mabua ya
ngano.
• Pakiti moja au mbili za dawa ya Coccid (hii inapatikana
katika maduka yote ya kilimo). Hata hivyo, utaratibu wa chanjo ni lazima
ukamilishwe.
• Chakula cha vifaranga kiwe kimezalishwa na
watengenezaji wanaoaminika au ikiwezekana tengeneza mwenyewe kwa kufuata maelekezo ya wataalam.
imeandaliwa na Melkiory Magesa M (Afisa Ugani/Kilimo na mifugo)
No comments:
Post a Comment